Maisha
ya Mwanamume
Hapo awali, maisha ya mwanamume kawa rahisi
Kazi yake ni: kuilinda, kuitunza na kuiongoza jamii
Kwa makini, yeye kawa mshauri na muuguzi
Taifa kawa na ustawi, mwongozo wake mema maadili.
Ila leo, mfumo kabadilika, jina maendeleo
Ya Kizungu, mambo, macheo hadi machweo
Mila, desturi tokomea, Uafrika sahaulika
Wa kiume mwana, uume hana tena.
Hapo awali, mwana wa mume lake rika
Baada ya kazi, wake wenza wampe wosia
Tunza bibi hivi, vipi uisimamishe jamii
Fumbo, methali, semi - zamfunza mengi.
Elimu sasa ya Kizungu, huru jitawale mja
Vazi chaguo langu, hasemezeki wangu dada
Elimu hii sumu, pesa anazo – gari, madaraka
Atoa kutu – apendavyo - pasi kujali ndoa.
Hapo awali, ndoa adhimu, mfano wa kuigwa
Bwana bibi, dhambi adimu, kaepuka zinaa
Fungate safi, milele idumu, shemeji mmoja
Jalali bariki, kifaa sio butu, ofisi bila doa.
Sasa maisha sherehe, haina rika hii pombe
Waume wake, vijana tangamana na wazee
Sababu yake, ndugu - utajiri na uchochole
Hana mbele, kijana, hamtembelei shehe.
Nani gari lake kubwa, vazi jipya, majibwa
yabweka
Sauti kuu ya pesa, itakupa heshima, dharau utapata
Uchochole unapokupata, kombo waona wewe kengeza
Umaskini ukoma, marafiki na ndugu wamekutoroka.
Madaraka ulijisifia, sasa kazi kaisha, wote
wanakusengenya
Wamefunga nyumba, bibi ametoroka, tumbo limezoea njaa
Heshima imeshuka, tabasamu zimeisha, wakali wanadada
Kanisa haina hurumu, toa, toa, toa… kwa kukimbilia hamna.
Simu bubu, mbona usiiuze? makao vichochoro
Siku zote usiku, balaa lishe, maisha yako ovyo
Baya dudu, si mtu wewe, tamu pipa makombo
Mwana wa Adamu, kiwete, wakaribia mwisho.
Kitanzi, kamba shingoni, ndoto hii ina
mazimwi
Telezi miti, kinaya ng’o! leo kamwe hafi nyani
Sauti, kuu… mziki, ipo siku, kaja wako mwokozi
Safari, mui kawa mwema, neema tupu hii bahati.
Useremela, ujuzi na maarifa, ndogo karakana
Ndoa mpya, pombe sahaulika, sasa kawa kiwanda
Sala, shukrani daima, wanawake tamaa, zima
Pesa, haina tawala, nyenyekevu sasa tabia.
Wosia kwa vijana wa kiume, mashaka epuka
Siku zote wewe yatima, jikuze kila dakika
Maana yako unapozalisha, jifichie yako akiba
Majira, panda shuka, mwanamume ameokoka.
Comments
Post a Comment